Saturday, March 29, 2014

SALA YA MAMA NA MWANAE



5.6 Matendo ya Utukufu:
Kisha kufa na Kristu tafakari ya rozari yatufufua pamoja na Kristu; kuuonja utukufu wake anapofufuka na anapopapaa mbinguni, kuonja furaha pamoja na Mama Bikira Maria aidha wote waliosikia habari kwamba Yesu amefufuka na kumwona mzima tena. Uwe pamoja na Mama siku ya Pentekoste na umshudie Mama akipalizwa  mbinguni na kuwekwa Malkia wa mbingu na dunia. Twangojea ukamilifu wa Kanisa na ulimwengu mzima, wakati sisi wenyewe tunaitangazia dunia  nzima Injili.

5.7.Sala ya rozari ni mdundo wa maisha ya mtu. Kumtafakari Kristu kupitia Mama Maria. Kusali rozari ni kumkabidhi Bwana Yesu pamoja naye Mama Maria mizigo yetu yote.

Ahadi za Mama kwa wanaosali rozari:
(alizowakabidhi Mtakatifu Dominiko na Mwenye heri Alan)
1.Yeyote anayenitumikia kwa kusali rozari tutampa neema kadhaa nyingi na kubwa, tena basi za pekee.
2. Naahidi kwamba wote wanaosali rozari nitawalinda sana na kuwapa neema nyingi kabisa.
3.Rozari itakuwa kwao nguo ya kuwakinga wasiingie motoni, itakomesha mwenendo mbaya hatua kwa hatua, itawaponya mwelekeo wa kutenda dhambi, watashinda  uasi wa kukana kweli mbalimbali za Imani na maadili ya kimungu.
4.Rozari itaimarisha fadhila na maadili mbalimbali ya kimungu, itadumisha  na kustawisha  matendo mema, itawawezesha wenye kuisali watubu na kupata msamaha mwingi wa Mwenyezi Mungu.
5.Mtu yeyote anayejitoa na kujiweka kabisa mikononi mwangu kwa kuisali Rozari, kamwe sitamwacha afe katika hali ya dhambi ya mauti na wala hataonja moto wa milele.
6.Ninaahidi pia kwamba ajali mbaya wala mikosi haitamshinda mtu yeyote anayesali Rozari kwa ibada, huku akiyakumbuka na kuyatafakari matendo makuu ya kazi ya ukombozi ambayo rozari hukumbusha, kuhimiza na kumwezesha mtu ayatende katika maisha yake.
7.Yeyote anayefanya bidii ya kuisali rozari vema, na mara kwa, hakika atapokea sakramenti za Kanisa kabla ya kuyaacha makao haya ya muda.
8.Watu wanaosali rozari kadiri nilivyoagiza(yaani rozari nzima, kwa ibada kila siku) Mungu ataangaza nyoyo zao kwa nuru yake na kuwajaza neema zake wakati wangali wanaishi hapa duniani na saa yaa kufa kwa Mungu atawapokea mbinguni na kuwashirikisha tuzo na mastahili ya Watakatifu.
9.Nitawaondoa Toharani wale wote wanaojitahidi na kukazana kusali rozari kwa ibada.
10.Wana wa rozari waingiapo mbinguni tutawatunza kwa utukufu wa kiwango cha juu sana.
11.Kwa njia ya rozari niombeeni chochote name nitawapeni.
12.Katika shida zote, nitawasaidia kwa namna ya pekee wale wote wanaotangaza na kueneza rozari.
13.Mwanangu  Yesu amenikubalia kwamba, wale wote wanaotetea rozari iweze kusaliwa na kutumiwa, tutawapatia Malaika na Watakatifu wote wa mbinguni ili wawaombee katika maisha yao yote na katika saa yao ya kufa.
14.Wote wanaosali rozari ninawahesabu ni watoto wangu na ndungu za Mwanangu wa pekee, Yesu Kristu.
15.Kusali  rozari kila siku kadiri nilivyoagiza ni ishara ya kuitwa na Mungu Mwenyezi kuingia Mbinguni.

Namna ya kusali rozari.
Kumbuka .
Mafungu yote 20 ya Rozari ya Fatima, nay ale 7 ya Rozari ya Mateso Saba ya Mama Bikira Maria, yanaposaliwa mfululizo ile sehemu ya wali, yaani kuanzia Kanuni ya imani hadi Salamu Maria 3 za kuomba imani, matumaini na mapendo, husaliwa mara moja tu. Mafungu hayo lakini yakisaliwa kwa nafasi mbalimbali, yaaani mafungu ya Furaha pekee, mafungu ya nuru pekee, na kadhalika, hapo kila safari rozari huanzia na Kanuni ya Imani. Au na ile Baba yetu ya kwanza kabisa.
Matendo ya Furaha              =        Matendo ya Uchungu.
+Matendo ya Nuru              -          Matendo ya Utukufu.
Sala ziundazo rozari
1.Ishara ya msalaba: (mwanzo na mwisho)
Kwa jina la Baba na La Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.
2. Kanuni ya Imani:
Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, Mwumba  Mbingu na Dunia. Na kwa Yesu Kristu, Mwanae wa pekee Bwana wetu, aliyetungwa kwa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsio Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashuka kuzimu, siku ya tatu akafufuka katika wafu,akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi, toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa katoliki, Ushirika wa Watakatifu, maendeleo ya dhambi, ufufuko wa miili, uzima wa milele.
Amina.
3.Baba Yetu.
Baba Yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe. Ufalme wako ufike. Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni. Utupe leo mkate wetu wa kila siku.Utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea. Usitutie katika kishawishi, lakini utuopoe maovuni. Amina.
4.Salamu Maria;
Salamu Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe. Umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa  kwetu. Amina.
5.Atukuzwe Baba:

6.Waridi:(sala tatu pamoja:Sala ya Fatima ya kuombea wakosefu, sala ya Tobara kuombea marehemu,
Tuwasifu milele Yesu, Maria na Yosefu.
Ee Yesu utusamehedhambi zetu. Utukinge na moto wa milele. Uongoze roho zote Mbinguni, hasa wale wanaohitaji zaidi huruma yako.
Damu ya Kristu, iziokoe roho zinazoteswa Toharani, uzitie nuru ya uzima  wa milele.Amina.
Mama  na Mwana, mtujalie kuishi mnayosema, na kupata mnayoahidi.
Maandilizi ya Kiroho.
1.Kwa neema yako Mungu Mwenyezi(Sala ya Papa Yohane Paulo II)
K.Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho  Mtakatifu.
W.Amina.
K.Kwa neema yako Mungu Mwenyezi , imani na tafakari, tunaanza(naanza) sala hii ya rozari; safari yetu(yangu) ya kiroho pamoja na Bwana Yesu, Mama Maria na Malaika, ya kuja kwako Baba wa milele.
Tunapotafakari (ninapotafakari) matendo haya mateule ya kazi ukombozi, yaliyochaguliwa miongoni mwa matendo mengi  mengine, tunaomba(ninaomba) Mwenyezi Mungu ujaze mioyo yetu kwa furaha ya Krismas; Bwana Yesu nuru ya dunia, angaza ulimwengu mzima, Kanisa lako, Tohara na Limbo, na familia zote, nawe Mama yetu Bikira Maria utuombee wanao wote wanyonge na wakosefu neema ya kushiriki kikamilifu pamoja nawe raha na mateso ya Kristu na yako mwenyewe, hatimaye utukufu wa ufufuko, milele na milele.
W.Amina.
2.Tunakuabudu Mungu mmoja.
K.Baba wa mbinguni, Bwana Yesu Kristu, Mungu Roho Mtakatifu mfariji.
W.Tunakuabudu Mungu mmoja katika Umoja wa Utatu Mtakatifu na kukiri pamoja na Malaika.
Mtakatifu, Mtakatifu,Mtakatifu, Bwana Mungu wa Majeshi Mungu uliyekuwepo, uliyepo na unayekuja.
Nawe Bikira Maria, Mama wa Mungu, Malkia wa Mbingu na dunia na wa viumbe vyote, pokea pia salamu yetu wanao. Malaika na Watakatifu wote wa Mbinguni, karibuni. Twaomba, iwapendeze nyote, kwa namna ya pekee kusali pamoja nasi, wana wenu tuliokusanyika hapa leo.
Tunakuomba pia, Mama yetu Bikira Maria ikupendeze pamoja  na wakazi wa mbinguni kuwahudumia watoto wale ambao wanatamani kuwa hapa lakini wameshindwa kufika. Kwa pamoja tusaidieni tuweze katika nafasi Mwenyezi Mungu jinsi anavyostahili, anayeishi na kutawala milele. Amina.
3.Kumkaribisha Roho Mtakatifu.
K.Karibu Mungu Roho Mtakatifu Mfariji, utuangaze na ututie nguvu mpya tuweze kuadhimisha vema ibada hii ya rozari takatifu.
Wimbo/Sala:
Kiitikio:Uje Roho Mfariji, shusha kwetu vipaji,  Roho Mungu njoo.
K.1.Tushushie hekima, tukupende daima, Roho Mungu njoo.
2.Tunaomba akili, tufahamu imani, Roho……….
3.Tusaidie kwa ushauri, tuchague vizuri, Roho………..
4.Nguvu iwe tayari, tushindane hodari , Roho………..
5.Utujaze elimu, mafundisho yaelee, Roho……..
6.Tuwashie ibada, na uchaji wa Mungu, Roho……..
4.Kuomba toba.
K.Ndungu zangu sote hapa tu wakosefu. Tukisema kwamba hatuna dhambi twazidanganya nafsi zetu wala ukweli haumo ndani yetu. Papo hapo Mungu ni mwingi wa huruma, hana hasira. Hivyo, tukiri sasa makosa yetu, tumwombe msamaha kwa ajili ya dhambi zetu wenyewe, dhambi za ulimwengu wote na hasa wale wasiomkiri Mungu, wasiokumbuka kabisa kutubu aidha walio mahututi, pia kwa ajili ya roho walioko Toharani na watoto wachanga waliokufa bila kubatizwa.
K.Nakuungamia Mungu Mwenyezi,
W.Nanyi ndungu. Kwani nimekosa mno ,kwa mawazo, kwa maneno,  kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu . Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndiyo maana nakuomba Maria mwenye heri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndungu zangu. Niombee kwa Bwana Mungu wetu.
Amina.
K.Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu, atufikishe Kwenye uzima wa milele.W.Amina.
5. Kujikabidhi kwa Mama Bikira Maria.(rejea kwenye ukarasa wa mwanzo katika blogi)
MATENDO YA ROZARI TAKATIFU NA LITANIA YA MOYO IMMAKULATA.
Rozari ya Fatima:Matendo ya Furaha:
Nia:Tunapokumbuka miaka 12 ya utoto wa Bwana Yesu tuombe Mungu atujalie amani na imani kwake kwa ajili ya Tanzania na ulimwengu.
Wimbo:Ahadi imetimia.
1.Ahadi imetimia, furaha ya Noeli,
Ndiyo ya Nazareti yafuta ya Edeni,
-Nuru imeingia ulimwenguni, amani kwa watu wenye mapenzi mema.
2.Mtamaniwa wa Israeli, Mwokozi wa dunia, wanamfia wachanga, wazee wamsujudia.
-Anapokimbilia kule Misri, aiambia Afrika: Amani kwako.
3. Siku tatu hekaluni, amefunza Viongozi, majilio yake mawili, uchambuzi wa ajabu.
- Leo Nuru ni kondoo wa kuchinjwa, kesho wa wote Hakimu mtukufu.
Matendo ya Furaha.
1.Malaika anampasha habari Maria kwamba atakuwa Mama wa Mungu
-Tumwombe Mungu atujalie unyenyekevu.
Waridi:Baada ya kila fungu(fumbo) la rozari husaliwa
-Tuwasifu milele Yesu, Maria na Yosefu.
-Ee Yesu, utusamehe dhambi zetu, utukinge na moto wa milele. Ongoza roho zote mbinguni, hasa za wale wanaoitaji zaidi huruma yako.
-Damu ya Kristu, iziokoe roho zinazoteswa toharani, izijalie nuru ya uzima wa milele. Amina
-Mama na Mwana, mtujalie kuishi mnayosema na kupokea mnayoahidi.
Amina.
2. Maria anakwenda kumtembelea Elizabeth.
-Tumwombe Mungu atujalie  mapendo ya jirani
Waridi:Tuwasifu……….
3.Yesu anazaliwa Betlehemu.
-Tumwombe Mungu atujalie moyo wa ufukara
Waridi:
4.Yesu anatolewa  hekaluni.
-Tumwombe Mungu atujalie usafi wa moyo
Waridi:
5.Maria anamkuta Yesu hekaluni
-Tumwombe Mungu atujalie kuwatii wakubwa wetu.
Waridi:Tuwasifu……
WKW.Husaliwa kila baada ya matendo matano, na mwisho wa Rozari ya Mateso 7:

Rozari ya Fatima:Matendo ya Nuru.
Nia:Tunapokumbuka miaka mitatu ya mwisho ya ujana wa Bwana Yesu tuliombee Kanisa, tohara na Limbo, pia roho sugu wamrudie  Mungu.
Wimbo:Walipoona nuru
(i)Walipoona nuru ya Baba,/  Wakaisikia na sautin yake,…
Petro alikiri:/ Ni vema sisi kuwapo hapa!
(ii)Sasa tekeni, asema Yesu, /mpekeeni mkuu wa meza
Wakashangaa: / Siyo maji, ni divai njema!
(iii)Yesu mtoni Yordani, / Roho ashuka, Baba anena;
“Msikieni yeye” /Mwanzo mkuu wa ubatizo.
(iv)Kuleni, huu mwili wangu, / Kunyweni, Hii damu yangu,
Alisema Yesu. /Kaeni katika pendo langu.
(v)Na walio gizani tubuni, / Ufalme wa Mungu u karibu, Yesu atangaza, /ndimi Nuru ya ulimwengu.
Matendo ya Nuru.
1.Yesu anabatizwa mtoni Yordani.(Mt. 3:15)
Yesu alimwambia Yohane Mbatizaji:
Ukubali hivi sasa, unibatize, tupate kutimiza haki yote.
-Tuombe neema ya kumtii Mungu kuliko chochote.
Au: Mbingu zikafunguka; Baba anena:
Huyu ni mwanangu mpendwa wangu.
Na Roho Mtakatifu ashuka mfano wa njiwa.
-Tuombe nuru tuukiri Utatu Mtakatifu na kushiriki vema kazi ya ukombozi.
Waridi: Tuwasifu……..
2.Yesu anageuza maji kuwa divai katika harusi ya Kana.
(Mt. Yoh. 2.3, 5)
Mama  Bikira Maria alimwambia Yesu: Hawana divai.
Kisha akawaambia watumishi: Lolote atakalowaambia fanyeni.
-Tuombe neema  ya kumheshimu , kumsikiliza na kumtii Mama wa  Mungu siku zote.
Waridi….
3.Yesu anahubiri(Mt.4:12,17)
Yesu alikwenda  mpaka Galilaya, akaanza kuhububiri na kusema;
Tubuni, kwa maana ufalme wa  Mbingu umekaribia.
-Tuombe neema ya kuweka miyoni mwetu kila neno litokalo kwa Mungu na kulitenda.
Au: Tuombe tumpokee kwa imani Kristu, Nuru ya dunia na Mkombozi wetu.
      Waridi…
4.Yesu anageuka sura.(Mt. 17:5)
Mungu alinena kutoka mbinguni Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, Ninayependezwa naye, msikieni yeye.
-Tuombe neema ya kumsikiliza Yesu na kutenda asemayo, atujalie nuru ya kumwona uso kwa uso milele yote.
                   Waridi…
5.Yesu anaweka Ekaristi Takatifu(Mt. 16,26-28, Lk.22:17-20).
Katika karamu ya mwisho Yesu aliwaambia Mitume wake,  Huu ndio mwili wangu, uleni. Hii ndiyo damu yangu, inyweni. Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi.
-          Tuombe neema: Kamwe tusiikufuru Ekaristi Takatifu, nuru ya pendo la Yesu,sadaka timilifu.
-          Waridi…..WKW.
Rozari ya Fatima:Matendo ya Uchungu.
Nia:Tunapokumbuka wiki ya mwisho ya maisha yake Bwana Yesu tuwaombee wagonjwa,wafungwa, wasafiri na wenye shida mbalimbali za maisha.
Wimbo:Kikombe cha moto.
(i)Kwa ajili yetu, umekwenda ile njia, ya ghadhabu yake Mungu.
(ii)Kwenye ile bustani, iliyofumbata msiba, ‘imetoka jasho la damu.
(iii)Ukakumbwa upweke, mijeredi ukapigwa, taji la miiba’kavikwa.
(iv)Kikombe cha moto kile, msalaba ukabebeshwa, mtini ukaangikwa.
(v)Mtu wa masikitiko, huzuni hiyo ya kwako,’tutie nuru na toba.
Matendo ya Uchungu.
1.Yesu anatoka jasho la damu.
- Tumwombe Mungu atujalie sikitiko timilifu.
         Waridi:Tuwasifu……
2.Yesu anapigwa mijeredi.
-Tumwombe Mungu atujalie kuacha dhambi za uchafu.
Waridi.
3.Yesu anatiwa miiba kichwani.
-Tumwombe Mungu kushinda kiburi
Waridi.
4.Yesu anachukuwa msalaba.
-Tumwombe Mungu atujalie kuvumilia taaba.
Waridi….
5.Yesu anakufa msalabani.
-Tumwombe Mungu atujalie kuwapenda Yesu na Maria.
Waridi…WKW

Rozari ya Fatima: Matendo ya Utukufu.
Nia:Tunapoifurahia  Pasaka ya Bwana Yesu na kipindi kizima baada ya ufufuko wake tuombee familia, wajane na yatima, wanafunzi na wakimbizi.
Wimbo:Uhai umepatikana.
(i)Bendera za kifalme, kokote zapepea , Uhai ‘mepatikana.
(ii)Utatu Mtakatifu, sifa tunakuimbia Kristu mzima kafufuka.
(iii)Kristu mbinguni kapaa, kulia umekalia mshindi wa mauti.
(iv)Hongera Mama  Maria, Mbinguni umepalizwa roho pamoja na mwili.
(v)Mbinguni Mungu yu Baba, Mwana ndiye Mfalme, Mama na Malkia ni wewe.
Matendo ya Utukufu.
1.Yesu anafufuka.
-Tumwombe Mungu atujalie kugeuka watakatifu.
Waridi:Tuwasifu…..
2.Yesu anapaa mbinguni.
-Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu
Waridi.
3.Roho Mtakatifu anawashukia Mitume.
-Tumwombe Mungu atujalie bidii katika dini yetu.
Waridi.
4.Bikira Maria anapalizwa mbinguni.
-Tumwombe Mungu atujalie kudumu katika njia njema.
5.Bikira Maria anawekwa  Malkia mbinguni.
-Tumwombe Mungu atujalie kufa vema.
Waridi….WKW.
Rozari ya Mateso saba ya Mama Bikira Maria.
Wimbo:Mama pale msalabani.
(i)Mama  pale msalabani, macho yatoka machozi, akimwona Mwanae.
(ii)Kweli vile akilia, uchungu kama upanga ukampenya moyowe.
(iii)Mwenye moyo mgumu nani, asimhurumie basi Mama mlilia Mwana?
(iv)Ewe Mama mtakatifu, usulibiwe na Yesu, moyo wangu wa dhambi.
(v)Nae Mwokozi niteswe, madonda nigawiwe, pamoja na Mkombozi.
(vi)Nisimame msalabani, niwe name wako mwenzi, wa uchungu na msiba.
Mateso 7.
(Kila teso hutanguliwa na sala fupi ifuatayo)
Majonzi na mateso ya Mama Maria wa Yesu hayana mfano.
1.Mzee Simeoni aliagua kwamba Bikira Maria atachomwa upanga moyoni.
-Tuombe neema ya kuvumilia mateso. Mama wa mateso, utuombee
Waridi:Tumsifu……
2.Mama Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Yesu asiuawe na Herodi.
-Tuombe neema ili mioyo yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso, utuombee.
Waridi.
3.Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa muda wa siku tatu,
-Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso, utuombee.
Waridi.
4.Bikira Maria alikutana na Yesu katika njia ya msalaba.
-Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote .
Mama wa mateso,  utuombee
Au:Tuombe neema nasi tubebe hodari misalaba yetu siku zote
Mama  wa mateso, utuombee.
Waridi
5.Bikira Maria alimwona Mwanae akitundikwa msalabani;
Akasimama chini ya huo msalaba kwa muda wa masaa sita.
-Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Mama  Maria.
Mama wa mateso ,utuombee.
Waridi.
6.Mama Maria alimpokea Mwanae na kumpakata miguuni pake kisha shushwa msalabani.
Alishiriki kikamilifu mateso ya Mwanae kwa ajili ya dhambi za wanadamu.
-Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso, utuombee.
Au Tuombe neema ya kumpokea Yesu wa Ekaristi Takatifu kwa ibada na uchaji sikuzote.
Mama wa mateso, utuombee.
Waridi.
7.Mama Maria alirudi kwa majonzi nyumbani kisha kumzika Mwanae Yesu.
-Tuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria katika mateso yetu.
Mama wa mateso, utuombee.
Waridi….WKW 
Litania ya Moyo Immakulala wa Maria.
Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie
          Kristu utuhurumie
Kristu utuhurumie
          Bwana utuhurumie
Baba wa mbinguni, Mungu     utuhurumie
Mwana, Mkombozi wa dunia, Mungu    utuhurumie
Roho Mtakatifu, Mungu     utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu Mmoja     utuhurumie
Moyo Immakulata wa Maria ulioshiriki kikamilifu kazi ya ukombozi ya Mwanae    utuombee.
Moyo unaochomwa kila siku kwa kuona roho nyingi zinateketea  utuombee.
Moyo Immakulata uliojaa upendo kwa binadamu  utuombee.
Moyo Immakulata unaohuzunika kwa dhambi za binadamu   utuombee
Moyo Immakulata unaotamani kutulizwa na binadamu kwa njia ya rozari Takatifu    utuombee
Moyo Immakulata unaotamani kuvuta roho zote ziingie katika Ufalme wa mbingu.
Moyo Immakulata unaosikiliza kilio cha watoto wake dhaifu na wanyonge.  Utuombee.
Moyo Immakulata ambao uko tayari kumfariji kila anayemkimbilia    utuombee.
Moyo Immakulata unaoalika siku hadi siku.
“Njoni mkamiminiwe neema zitokazo katika Moyo huu”   utuombee
Moyo Immakulata unaoomba daima,
“Fanyeni malipizi mahali mahali pa wakosefu wote”   utuombee.
Moyo Immakulata unaokumbusha daima ,
“Waombeeni  marehemu Toharani bwanaoteseka na ambao hakuna anayewakumbuka”    utuombee.
Moyo Immakulata unaoagiza kwa upendo;
“Waombeeni pia watoto wachanga wanaokufa bila ubatizo    utuombee.
Moyo Immakula unaohimiza daima:” Uombeeni ulimwengu amani ya kweli pamoja na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu”    utuombee.
Moyo Immakulata unaohiza daima:”Liombeeni Kanisa na hasa viongozi wake na Watendakazi wote Mama Maria”   utuombee
Sehemu ya pili.
Moyo safi wa Maria, baada ya moyo wake Mungu mwenyewe   utuombee.
Moyo safi  wa Maria, Ee chombo cha Roho Mfariji      utuombee.
Moyo safi wa Maria, goroto la Utatu Mtakatifu      utuombee.
Moyo safi wa Maria, makao ya Neno la Mungu   utuombee.
Moyo safi wa Maria , mkingiwa dhambi tangu kuumbwa.   Utuombee.
Moyo safi wa Maria, unaofurika  neema      utuombee.
Moyo safi wa Maria,  mbarikiwa  kati ya mioyo yote.  Utuombee.
Moyo safi wa Maria, kiti cha enzi cha utukufu      utuombee.
Moyo safi wa Maria, bahari ya unyenyekevu       utuombee.
Moyo safi wa Maria, sadaka ya mapendo    utuombee.
Moyo safi wa Maria, uliosulubishwa wakati  umesimama chini ya msalaba.  Utuombee.
Moyo safi wa Maria, mtuliza wenye huzuni.  Utuombee.
Moyo safi wa Maria, makimbilio ya wakosefu       utuombee.
Moyo safi wa Maria, matumaini yao wanaozimia.  Utuombee.
Moyo safi wa Maria, makao ya huruma    utuombee.
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia   utusamehe ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia   utusikilize ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, uondoaye dhambi za dunia     utuhurumie.
K.Moyo Immakulata, mpole na mpole na mnyenyekevu,
W. Utufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wa Yesu.
Tuombe, Mungu mwingi wa huruma, ili kuwajalia wakosefu wokovu na wanyonge makimbilio, umeufanya Moyo Immakulata wa Mama Maria ufanane sana na Moyo wa Yesu kwa wema na huruma zao.
Twaomba, utujalie nasi tunaoheshimu Moyo huu Immakulata mtamu na uliojaa upendo, tustahili kuishi katika kuifuhasa Mioyo miwili iliyoungana, ya Mama na Mwanae. Kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.
Sala za Mwisho
Kamwe hatukuachi.(Papa Yohane Paulo II)
Kamwe hatukuachi, Ewe rozari takatifu ya Mama Maria, Cheni itufungayo na Mungu, mkufu wa upendo utuungao na Malaika, mnara imara utukingao na maoteo ya shetani, bandari salama katika bonde kubwa la machozi. Usimpe shetani nyara za bure, zuia na uzime vita vyote duniani.
Ndiwe faraja yetu saa ya kufa, Ee Malkia wa rozari wa Pompei, Mama mpendelevu, kimbilio la wateswa, usifiwe popote, leo na daima, hapa dunia na huko mbinguni.
Amina.
Salamu Malkia.
Salamu Malkia, Mama mwenye huruma, uzima tulizo na matumaini yetu salaam. Tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva.
Tunakulilia, tukilalamika na kuhuzunika bondone huku kwenye machozi. Haya basi, Mwombezi wetu, utuangalie kwa  macho yako yenye huruma. Na mwisho wa ugeni huu utuonyeshe Yesu, Mzao mbarikiwa wa tumbo lako.
Ee mpole, ee mwema ee mpendevu, Bikira Maria. Amina.
KumbukKumbuka, Ee Bikira Maria mpole sana, haijasikilika bado hata mara moja, kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, aliyeomba msaada wako na maombezi yako. Kwa matumaini hayo nakukimbilia wewe, ee Mama, Bikira wa Mabikira. Ninakuja kwako, ninasimama mbele yako nikilalamika mimi mkosefu, ee Mama wa Neno la Mungu, usikatae maneno yangu, bali upende kuyasikia na kuyasikiliza. Amina.
Tunakimbilia.
Tunakimbilia ulinzi wako, ee Mzazi Mtakatifu wa Mungu usitunyime tukiomba katika shida zetu. Utuokoe siku zote kila tuingiapo hatarini. Ee Bikira mtukufu mwenye Baraka. Amina.
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.

No comments:

Post a Comment