Tuesday, September 5, 2017

Maisha ya Mtakatifu Papa Gregori Mkuu(Life of Saint Pope Gregori)

 
Mtakatifu Papa Gregori Mkuu alizaliwa Roma, Italia, mwaka 540  hivi katika familia ya ukoo maarufu ya Anicia, akiwa mtoto wa seneta Gordianus  na wa Silvia, ambao wanaheshimiwa kama watakatifu.Shangazi zake Emiliana na Tarsila, wakiishi nyumbani mwao kwa sala  na toba kama mabikira wa Kristo, walimtia pia hisia za Kikristo kweli. Kati ya mababu wake kulikuwa na Papa Felis II toka mwaka 483 hadi 492 na mwingine Papa Agapito I toka mwaka 535 hadi 536.Mtakatifu Papa Gregori alifariki Roma tarehe 12 Machi 604.

Alipokuwa na umri wa miaka 25 tu alifuata nyayo za baba yake katika shughuli za utawala na mwaka 572  alichaguliwa kuwa mkuu wa jiji la Roma. Kutokana na ugumu wa nyakati hizo, kazi hiyo ilimdai awajibike katika masuala mengi tofauti ikimuandaa kwa majukumu yake ya baadaye.
Kwa namna ya pekee alidumisha hisi ya kuwepo haja ya utaratibu na nidhamu katika mambo yote. Ndiyo sababu baadaye, akiwa papa, alihimiza maaskofu waendeshe shughuli zao kwa kufuata mfano wa uwajibikaji na utekelezaji wa sheria wa watawala wa kisiasa.

Hata hivyo maisha hayo hayakuweza kumridhisha. Kwa hiyo, baada ya muda mfupi aliyaacha, na akivutiwa na mfano wa Mtakatifu Benedikto wa Nursia, aligeuza nyumba yake mjini kuwa monasteri  na kujifanya mmonaki, halafu akajitahidi katika maisha ya sala na kutafakari Biblia  na maandishi ya mababu wa Kanisa. Pia alianzisha monasteri 6 katika kisiwa  cha Sicilia. Maisha hayo ya kuhusiana na Bwana tu yalimuandaa kutoa mafundisho yake bora na yalizidi kumvutia hadi mwisho, kama alivyoandika mara nyingi baadaye.

Lakini mapema, kutokana na sifa  na mang'amuzi  yake, Papa Pelagio II  alimfanya shemasi  akamtuma kama balozi  kwenye ikulu  ya Konstantinopoli, alipobaki miaka sita akiendelea kuishi kimonaki na wenzake kadhaa kati ya fahari za mazingira ya Kikaisari. Majukumu yake makuu yalikuwa kukomesha mabaki ya mabishano kuhusu ubinadamu  wa Kristo na hasa kupata msaada  wa Kaisari  dhidi ya uvamizi  wa Walombardi  nchini Italia. Hata miaka hiyo ilimuandaa kwa kazi zake za baadaye.

Aliporudi Roma,mnamo mwaka 586, akarejea monasterini, lakini Papa huyo alimfanya katibu  wake. Ilikuwa miaka migumu kwa mvua za mfululizo,mafuriko na njaa  mjini Roma na sehemu mbalimbali za Italia. Hatimaye tauni  ilifyeka watu wengi, Pelaji II akiwa mmojawao.

Hivyo tarehe 3 Septemba 590 alishangiliwa na wakleri,maseneta na umati  wa watu kwa kauli moja  awe Papa wa 64. Ndiye mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, ingawa hakutaka, hata akajaribu kukimbia, lakini bure. Ilimbidi akubali mapenzi ya Mungu, akaanza mara kuwajibika.

Mapema alionekana kuwa na mitazamo na maamuzi sahihi na kujitokeza kama mtendaji bora upande wa Kanisa na hata upande wa jamii na siasa (kwa sababu hiyo aliitwa "Mrumi wa mwisho"), ingawa alikuwa na afya mbovu, kiasi cha kulazimika mwishoni kubaki kitandani  kwa siku kadhaa. Hasa mafungo  makali ya kimonaki yalikuwa yamesababisha matatizo makubwa ya tumbo.

Tena sauti yake ilikuwa ndogo kiasi kwamba mara nyingi ilimbidi kumpa shemasi kazi ya kutangaza hotuba  yake alipoendesha ibada  makanisani kati ya waumini waliomheshimu sana kwa kumuona anawafanya wajisikie salama. Hotuba hizo zinaonyesha alivyotekeleza alichoandika: “Ni lazima mhubiri  achovye kalamu kalamu yake katika damu  ya moyo  wake; hapo ataweza kufikia masikio ya majirani wake”.
Aliwasiliana na viongozi wa nchi mbalimbali za Ulaya, na hasa wa kabila  la Wafaranki ambalo lilikuwa la kwanza kati ya yale ya Kijerumani kuingia Ukatoliki moja kwa moja tena lilijitokeza lenye nguvu kuliko yote.
Vilevile alifanikisha uongofu wa makabila ya aina hiyo yaliyoteka Uingereza, alipomtuma kama mmisionari Augustino wa Canterbury,priori wa monasteri  yake ya Mt. Andrea.

Alilinda pia Roma dhidi ya uvamizi wa Agilulf , mfalme wa Walombardi, lakini, kinyume na Kaisari aliyewaona ni washenzi  na wavamizi tu ambao wadhibitiwe au kuangamizwa, Gregori, kwa mtazamo wa kichungaji, alijenga nao uhusiano mpya ili kuwaleta kwenye Kanisa Katoliki  kutoka uzushi  wa Ario, kama alivyofanya pia na Wagoti wa Hispania  na walioendelea kufuata dini za jadi.
Akilenga amani  ya kudumu nchini Italia, kwa msaada wa Theodolinda,malkia Mkatoliki  wa Walombardi, alifanikiwa kwanza kusimamisha mapigano na Walombardi kwa miaka mitatu mwaka 598-601, na kuanzia mwaka 603 kwa muda mrefu zaidi.

Lakini mafanikio yake hayo, yaliyoandaa mengine kwa siku za mbele, yalimfanya achukiwe na watu wa Konstantinopoli.
Alipambana na matatizo mengine ya Italia, kama vile mafuriko, njaa, tauni, akisimamia kwa usawa masuala ya kijamii yaliyopuuziwa na wawakilishi wa kaisari. Kwa mapato ya mali ya Kanisa, aliyoisimamia vizuri na kwa kuzingatia haki, kati ya mambo mengine alilisha wenye njaa na kukomboa watumwa. Alishughulikia hata huduma ya maji.

Alirekebisha liturujia  ya Kiroma, akipanga matini ya zamani na kutunga mengine mapya, pamoja na kushughulikia muziki  wa ibada za Kilatini  ambao kwa heshima yake unaitwa wa Kigregori.
Vitabu vyake, hasa vya maadili  na vya ufafanuzi  wa Maandiko matakatifu unaolenga utekelezaji, barua 848 zilizotufikia pamoja na hotuba mbalimbali vinashuhudia kazi zake nyingi na ujuzi wake wa Biblia.

Pia aliandika maisha ya watakatifu kadhaa wa Italia walioishi si zamani sana, kama vile Benedikto wa Nursia ambaye tunamfahamu kwa njia hiyo tu. Ni kwamba rafiki  yake, Petro shemasi, alidhani wakati ule maadili yameharibika kiasi cha kuzuia upatikanaji wa watakatifu kama walivyotokea zamani. Basi, Gregori alimuonyesha kwamba, kinyume chake,utakatifu  unawezekana daima, hata katika mazingira  magumu. Masimulizi ya maisha yao yanaendana na hoja  za kiteolojia  zinazofafanua masuala mbalimbali.
Kitabu kingine kilichoacha athari kubwa ni "Mwongozo wa Kiuchungaji" kwa ajili ya maaskofu, ambao ulitafsiriwa mapema hata kwa Kigiriki na kwa Kisaksoni. Alikiandika mwanzoni mwa Upapa  wake akautekeleza mwenyewe. Humo anasisitiza ukuu  wa cheo hicho na majukumu yanayoendana nacho, ambayo yanadai askofu awe kielelezo kwa wote. Kwa ajili hiyo anapitia kwa makini aina mbalimbali za waumini na saikolojia  zao ili kuonyesha namna ya kuwasaidia. Hatimaye anakazia unyenyekevu wa kutojiona sawa mbele ya Hakimu mkuu kutokana na mafanikio fulanifulani: “Mtu anaporidhika kwa kutimiza maadili mengi, ni vema afikirie mapungufu yake na kujinyenyekesha: badala ya kuzingatia mema aliyofanya, ni lazima azingatie yasiyofanyika”. Kwake uchungaji ni “ars artium”, yaani sanaa  kuu kuliko zote.

Katika maandishi yake, hakukusudia kamwe kutoa mafundisho mapya, bali kuwa mwangwi  mnyenyekevu wa mapokeo  ya Kanisa. Alieneza mafundisho ya Augustino wa Hippo, akisisitiza kama yeye hali ya dhambi  ya binadamu, nafasi ya kwanza ya neema  katika wokovu  pamoja na imani  katika uteuzi wa watakaookoka uliofanywa na Mungu.

Pia alichangia ustawi wa fundisho la uwepo wa toharani.
Mtu huyo alikuwa wa ajabu kuliko kazi zake, akivutia kwa nguvu na upendevu wa tabia. Ndani mwake upana wa moyo na roho ya Kikristo vilitegemeza yote.Inawezekana kusema ndiye Papa wa kwanza kutumia mamlaka upande wa siasa pia, lakini bila kuweka pembeni majukumu yake ya kiroho kama mtu aliyeungana kweli na Mungu na hivyo aliweza kuona la kufanya. Kwake ilikuwa muhimu kila mmoja atafakari matukio ya maisha katika mwanga  wa Neno lake kwa sababu historia ya wokovu  haikumalizika zamani, bali inaendelea moja kwa moja hata katika nyakati ngumu kama zile alizopitia mwenyewe.

No comments:

Post a Comment