Leo tarehe 15 Septemba ni siku inayokumbukwa kila mwaka katika kukumbuka mateso ya Mama Bikira Maria. Wakati tukikumbuka Mama Bikira Maria wa Mateso hatuna budi kuzidi kushikamana naye katika mateso yetu katika maisha yetu mbalimbali.
Bikira Maria wa Mateso ni jina mojawapo linalotumika kumheshimu Mama wa Yesu kama mshiriki wa mateso na kifo cha Mwanae msalabani .
Liturujia ya Kanisa la Kilatini inaadhimisha kumbukumbu yake tarehe 15 Septemba, siku inayofuata sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba.
Ndivyo ilivyopangwa na Papa Pius X kwa Dunia nzima mwaka 1913, baada ya heshima hiyo kuenea sana katika ya Wakatoliki kuanzia karne ya 11.
Msingi wake ni hasa habari za Injili ya Luka (2:34-35,41-51; 23:27-31,55-56) na ya Yohane (19:25-27), lakini pia ile ya Mathayo (2:13) kuhusu mtoto Yesu alipokimbizwa ili asidhuhulike na mpango wa Mfalme Herode Mkuu .
Katika liturujia ya Neno,Misa ya siku hiyo ina sekwensya ya pekee, ambayo kwa Kilatini inayojulikana "Stabat Mater" ("Mama alisimama"), ambayo ndiyo maneno ya kwanza ya shairi hilo lenye muziki wa huzuni lakini mtamu.
Kama wanadamu tunayo mateso mbalimbali ambayo tunakuwa tunakumbana naye kupitia mfano wa mama yetu Bikira Maria na Mama wa Mkombozi wetu yatupasa kujifunza na kuendelea kumheshimu kwa kuwa alitesekana sana katika safari nzima ya Mwanae Yesu kwa lengo la kushiriki katika kumkomboa mwanadamu.
Rozari ya Mateso Saba ya Bikira Maria
Teso la Kwanza
Mzee Simeoni aliagua kuwa Moyo wa Mama Maria utachomwa kwa upanga.Tuombe neema ya kuvumilia mateso.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Pili
Maria na Yosefu walikimbilia Misri usiku ili kumficha Mtoto Yesu asiuawe na Herodi.Tuombe neema ili miili yetu iwe kimbilio lake Yesu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Tatu
Mama Maria aliona uchungu sana Mtoto Yesu alipopotea kwa siku tatu.Tuombe neema ya kudumu na Yesu mioyoni mwetu.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Nne
Mama Maria aliona uchungu sana alipokutana na Mwanae Yesu katika njia ya Msalaba.Tuombe neema ya kudumu na Yesu siku zote.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Tano
Mama Maria aliona uchungu sana alipomwona Mwanae Yesu akisulibiwa Msalabani.Tuombe neema ya kufa mikononi mwa Yesu na Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Sita
Mama Maria aliona uchungu sana alipopakata maiti ya Mwanae Yesu baada ya kushushwa Msalabani.Tuombe neema ya kutotenda dhambi.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Teso la Saba
Mama Maria aliona uchungu sana aliporudi nyumbani baada ya kumzika Mwanae YesuTuombe neema ya kitulizo kwa Mama Maria.
Mama wa mateso utuombee.
Baba Yetu ……… Salamu Maria x7. Atukuzwe Baba ……
Mateso na majonzi ya Mama Maria hayana mfano.
Litania ya Mateso Saba ya Mama Bikira.
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Mungu Baba wa Mbinguni, Utuhurumie
Mungu Mwana, Mkombozi wa dunia Utuhurumie
Mungu Roho Mtakatifu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu MMoja Utuhurumie
Maria Mtakatifu Utuombee (iwe kiitikio)
Mama wa Mkombozi wetu,
Mama mwenye mateso,
Malkia wa mashahidi,
Mama wa wenye uchungu,
Mfariji wa wenye taabu,
Msaada wa wenye shida,
Mlinzi wa wenye upweke,
Nguvu ya dhaifu moyoni,
Makimbilio ya wakosefu,
Afya ya wagonjwa,
Matumaini ya wanaozimia,
Kwa ajili ya ufukara wako ulioona pangoni Bethlehemu, - Utusaidie ee Mama wa mateso (iwe kiitikio)
Kwa ajili ya mateso yako uliyoona katika uaguzi wa Simeoni,
Kwa ajili ya taabu zako ulizopata katika safari ya Misri,
Kwa uchungu wako, Mwanao alipopotea,
Kwa ajili ya huzuni yako Mwanao alipodhulumiwa,
Kwa ajili ya hofu yako Yesu alipokamatwa,
Kwa ajili ya uchungu wako ulipokutana na Yesu katika njia ya Msalaba,
Kwa ajili ya mateso ya Moyo wako aliposulibiwa,
Kwa ajili ya mateso yako makali Yesu alipokufa,
Kwa ajili ya kilio chako juu ya Mwanao mpenzi,
Kwa ajili ya uchungu wako penye kaburi la Mwanao,
Kwa ajili ya upweke wako baada ya maziko ya Mwanao,
Kwa ajili ya uvumilivu wako katika shida zote,
Katika uchungu wetu wote,
Katika ugonjwa na mateso,
Katika huzuni na shida,
Katika umaskini na upweke,
Katika mahangaiko na hatari,
Katika vishawisho vyote,
Katika saa ya kifo chetu,
Katika hukumu ya mwisho,
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusamehe ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusikilize ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utuhurumie.
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Bwana utuhurumie – Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie.
Baba Yetu ….
Utuombee, ee Mama wa Mateso
Tujaliwe kupewa ahadi za Kristo.
TUOMBE: Ee Bwana Yesu Kristo, utusaidie sasa na saa ya kifo chetu msaada wa Bikira Maria Mama yako, ambaye moyo wake mtakatifu ulichomwa na upanga wa mateso ulipoteswa na kufa msalabani. Unayeishi na kutawala milele na milele. Amina.
Sala kwa Mama Bikira Maria Katika Ukiwa wake
Nakusikitikia sana Mama Mtakatifu Maria kwa sababu ya ukiwa wako mkuu. Uchungu wako ulikuwa mkubwa sana ulipotazama mateso na kifo cha Mwana wako mpenzi. Muda ule uliweza kutuliz kidogo kwa sababu ya kumwona angali hai. Lakini je, baada ya kufa na kumzika? Sasa wewe ni mkiwa mkubwa mno! Uh, ukiwa wa pekee, uniombee mimi ninayempoteza mara nyingi kwa dhambi zangu. Unijalie nisimpoteze tena Yesu wangu kwa ubaya wa uvivu wangu, bali nimtumikie kiaminifu duniani hapa ili nimwone na kumfurahia milele mbinguni. Amina.
Sala ya Majitoleo Kwa Mama Wa Huzuni
Mama Mtakatifu, Mama wa Mungu na Malkia wa Mashahidi, leo nakuchagua Wewe uwe mfano wangu, mkingaji na mteteaji wangu. Naweka roho fukara katika moyo wako uliotobolewa na panga nyingi za mateso. Unipokee mimi niwe mtumishi wako wa pekee na mshiriki wa mateso yako. Nijalie nguvu niwe daima karibu na msalaba ule alikosulibiwa Yesu. Nakutolea nafsi yangu na mali yangu yote. Pokea kila tendo langu jema ukalisindikize kwa Mwanao, Mama, nifanye nistahili kuitwa mtumishi wa Maria, Simama karibu yangu katika matendo yangu yote ili yafanwe kwa sifa ya Mungu. Ulivyosimama karibu kabisa ya Mwanao alipokufa msalabani uwe karibu nami saa ya kufa kwangu. Nijalie niweze kutaja jina lako na la Mwana wako nikisema: “Yesu, Maria na Yosef mnisaidie saa ya kufa kwangu. Yesu, maria na Yosef, naomba nife kwa amani kati yenu!” . Amina.
Sala Kwa Mama Wa Uchungu Kuomba Neema ya Pekee
Ee Mama mbarikiwa na Bikira mwenye uchungu, Malkia wa Mashahidi, uliyesimama chini ya msalaba na uliyemtazama Mwana wako akifa, unitazame kwa huruma ya kimama ninayekusikitikia. Kwa sababu ya upanga uliochoma moyo wako, kwa mateso ya maisha yako nakuomba uniangalie kwa wema ukasikilize maombi yangu. Nakuomba, ee Mama, uniombee daima kwa Mwana wako, najua hawezi kukuvyima wewe kitu chochote. Basi, ufanye, Moyo wa Mwanao ukubali kunijalia ombi langu hili …………………(taja ombi lako).
Maana nitamkimbilia nani katika mahitaji na misiba yangu isipokuwa kwako, ee Mama wa huruma? Wewe hasa unaweza kutusaidia sisi tulio bado katika bonde la machozi kwa sababu ulishiriki mateso ya Mwanao kutukomboa. Umtolee Yesu tone moja la Damu yake takatifu. Umkumbushe ya kuwa wewe ni matumaini, furaha na maisha yetu ukanipatie jambo ninalokuomba kwa Yesu Kristo, bwana wetu. Amina.
No comments:
Post a Comment