Yohana mbatizaji alikuwa mwana wa Mtakatifu Zakaria kuhani na mkewe , Mtakatifu Elizabeth (Luka 1: 5-25) .
Hizo zilikuwa nyakati ambapo Herode, akiwa mtawala mdogo wa Galilaya, chini ya dola ya Warumi . Herode alimkamata Yohana na kumuweka jela, kwa kuwa Yohana alimkemea na kumsema wazi wazi kutokana kitendo cha Herode kumuacha mkewe, aliyeitwa Phasaelis ( binti wa Mfalme Aretas wa Nabataea, sasa Jordan ) na kumuoa Herodia ambaye alikuwa mke wa nduguye (Herode Philip I) .
Herodia alimchukia Yohana, kwa kuwa alikuwa akikosoa jambo hilo, bila kificho. Herodia kwake aliona fahari kuolewa na Herode.
Herodia alikuwa na binti aliyemzaa katika ndoa yake ya awali aliyeitwa Salome.
Mfalme Herode alipoandaa sherehe kubwa ya kukumbuka kuzaliwa kwake, alialika wageni wengi na katika sherehe hiyo, binti wa Herodia (Salome) alicheza vizuri mno mbele za Mfalme na wageni. Mfalme akaamua kumpa zawadi, akamwambia Salome aombe chochote naye angempa. Binti yule aliamua kumuuliza mama yake, kitu gani aombe kwa mfalme.
Herodia akamwambia aombe kichwa cha Yohana Mbatizaji, ili kusudi aendelee kuishi kwa raha.
Mfalme Herode alipoambiwa kuwa yule binti ameomba kichwa cha Yohana Mbatizaji, alipata wakati mgumu mno, lakini kwa kuwa alikwisha ahidi kwa kiapo kuwa chochote kile akitakacho atampa, basi hakuwa na njia nyingine, akaamuru Yohana Mbatizaji akatwe kichwa na aletewe yule binti.
Ndipo, Yohana mbatizaji akakatwa kichwa na kikawekwa katika sinia, na kupelekwa kwa binti wa Herodia. ( Mathayo 14:1-12 )
Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji, waliuchukua mwili wake, wakauzika huko Sabaste (sasa Nablus -West Banks).
Herodia akakizika kichwa cha Yohana Mbatizaji kwa kificho. Lakini mwanamke mmoja ambaye aliitwa Joanna, aliyekuwa mke wa mmoja wa watumishi katika kasri ya Herode alimuona. Akachukua kichwa hicho na kukizika katika mlima wa mizeituni.
Maajabu mengi yalitokea yakipelekea kugunduliwa mahali kichwa hicho kilipozikwa, na mwisho mabaki ya kichwa hicho kupelekwa katika kanisa la San Silvestro huko Roma Italia.
*Watakatifu wengine wa leo ni*
Mt. Sabina
Mt. Adelphus
Mt. Basilla
Mt. Candida
Mt. Edwold
Mt. Euthymius
Wt. Hypatius na Andrew
Mt. Medericus
Wat. Nicaeas na Paul
Mh. Richard Herst
Mt. Sebbi
Mt. Velleicus