Mtakatifu Paulo wa Msalaba, ambaye jina lake la awali lilikuwa Paolo Francesco Danei, alizaliwa Ovada nchini Italia mnamo tarehe 3 Januari 1694 na inasemekana alifariki kwenye mji wa Roma tarehe 18 Oktoba 1775.
Mtakatifu Paulo wa Msalaba alikuwa padri mwanzilishi wa shirika la Mateso yaani Wapasionisti.Heshima yake iko juu ndani ya Kanisa Katoliki tangu tarehe 29 Juni 1867 hasa alipotangazwa na Papa Pius IX.
Akiwa na umri wa miaka 19 alipiga hatua kubwa, hata akaita kipindi hicho kuwa cha “uongofu wake”; kilikuwa na dalili za utakaso wa KiMungu wa hisia.
Kuanzia hapo Mtakatifu Paulo wa Msalaba alizama katika mafumbo yalipitia vipindi vitatu. Cha kwanza kilichukua miaka 12, ambapo aliinuliwa ngazi kwa ngazi hadi muungano unaotegeuza. Cha pili kilichukua miaka 45, ambapo aling’amua kwa dhati ya pekee maisha ya malipizi. Cha tatu kilichukua miaka 5, ambapo nderemo ziliongezeka kadiri alivyokaribia mwisho wa maisha yake, ingawa majaribu nayo yaliendelea.
Katika kipindi cha kwanza, baada ya usiku wa hisia na tabu zake, akiwa amejaliwa kuzama katika mafumbo, alidumu saa tatu au nne mfululizo katika sala ya moyo, jumla saa saba kwa siku. Kwenye umri wa miaka 24 alijaliwa sala ya kutoka nje ya binafsi alipopokea mianga mikubwa kuhusu mafumbo ya imani na njozi zilizomjulisha anavyotakiwa kuanzisha shirika la malipizi. Wakati huo alijaliwa pia njozi ya Utatu mtakatifu , ya mbinguni na ya motoni, akaona kana kwamba imani imekuwa jambo wazi.
Alipata utakaso wa Kimungu wa roho kwenye umri wa miaka 26, hasa wakati wa mfungo wa siku 40 aliposikia maneno ya kishetani dhidi ya Mungu yaliyomchoma moyo na roho. Utakaso huo ulimalizika kwa kuzama katika mateso ya Yesu aliyojipatia kwa njia ya upendo. Mwenyewe aliandika, “Roho ikiwa imezama yote katika upendo safi, pasipo utafiti, ila kwa imani tupu na safi kabisa inajikuta, inapompendeza Mungu aliye wema mkuu, imezama sawasawa katika bahari ya mateso ya Mwokozi” na kuona “kwamba mateso ni kazi ya upendo tu”. Tangu hapo sala yake ikawa kuvaa mateso ya Yesu na kujiachilia azamishwe katika umungu wake.
Kabla ya kufikia umri wa miaka 31 alijaliwa muungano unaotugeuza ulioendana na ishara ambazo pengine zinaudhihirisha kwa hisi (njozi na kupewa pete ya dhahabu iliyochongwa ionyeshe vyombo vya mateso).
Tunapaswa kuzingatia alivyoufikia mapema hivi muungano wa dhati na Yesu msulubiwa, na alivyotakiwa kuishi bado miaka 50 na kuanzisha shirika la malipizi, tusije tukashangaa kumuona baadaye kwa miaka 45 katika tabu kubwa za rohoni na upweke mchungu, ambapo kwa nadra tu Bwana alimjalia kupumua kidogo. Hakunyimwa tu faraja za kihisia, bali ni kana kwamba imani,tumaini na upendo vilipatwa visimng’ae. Alidhani ameachwa na Mungu kwa haira.
Vishawishi vya kukata tamaa na huzuni vilimlemea. Hata hivyo katika jaribu hilo la muda mrefu alionyesha subira kubwa, kujiachilia kikamilifu katika mapenzi ya Mungupamoja na wema mkubwa kwa wale waliomkaribia. Siku moja alimuambia kiongozi wake wa Kiroho, “Kama wangeniuliza muda wowote ninafikiria nini, naona ningeweza kujibu roho yangu inajihusisha na Mungu”. Ilikuwa hivyo hata alipojiona hana tena imani, tumaini na upendo: “Naona haiwezekani kuacha kumfikiria Mungu, kwa kuwa roho yangu imejawa naye, nasi sote tumo ndani mwake”.
Alipokuwa akipitia barabara za Roma na kulia, “Kutoka njia ya Paulo, utuopoe, Ee Bwana”, aliweza kupumua tu upande wa Mungu. Kwa miaka 45, usiku na mchana, sala yake chungu, ya kishujaa, isiyokoma, ilimtafuta kwa ari kwa niaba ya watu aliokuwa anateseka kwa ajili yao. Hivyo alitekeleza maneno ya Mwalimu “ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu sikuzote, wala wasikate tamaa” (Lk 18:1).
Paulo aliandika tena, “Tabu ndogondogo za mwili au za roho ndiyo vidato vya kwanza vya ile ngazi ndefu takatifu inayopandwa na watu bora na wakarimu. Hao wanapanda hatua kwa hatua hadi kufikia kidato cha mwisho. Huko juu wanakuta uchungu safi kabisa, usiochanganyikana hata kidogo na faraja toka mbinguni wala duniani. Nao wakiwa waaminifu wasijitafutie faraja yoyote, watavuka toka huo uchungu safi hadi upendo safi wa Mungu usiochanganyikana na chochote kingine. Lakini wanaofikia hatua hiyo ni wachache sana… Wanajiona kana kwamba wameachwa na Mungu, kwamba yeye hawapendi tena, amewakasirikia… Nikiruhusiwa kusema hivi, kidogo ni kama adhabu ya kumkosa Mungu milele, ni teso ambalo uchungu wake hauna mfano. Lakini mtu akiwa mwaminifu anakusanya hazina isiyopimika! Dhoruba zinapita na kwenda zake, kumbe yeye anakaribia muungano halisi, mtamu na wa dhati na Yesu msulubiwa, ambaye anamgeuza ndani mwake na kumlinganisha naye”.
No comments:
Post a Comment