Mtakatifu Ambrosi wa Milano alizaliwa mwaka 340 hivi katika familia ya Kikristo ya Dola la Roma katika mji uitwao Trier, akakulia huko.Mtakatifu Ambrosi wa Milano(Aureli Ambrosi) alikuwa askofu wa Milano kuanzia mwaka 374 hadi kifo chake.Maandiko yanatueleza Mtakatifu Ambrosi wa Milano ndiye aliyemuongoa na kumbatiza Agostino wa Hippo. Ambrosi aliendelea na ugavana hadi mwaka 374 alipochaguliwa askofu wa Milano.
Na vitu vilivyomfanya mpaka kuwa Askofu ni kwamba, baada ya kifo cha askofu Ausensi aliyefuata uzushi wa Ario , Ambrosi alikuwa amefika kanisani ili kutuliza ghasia kati yana Wakatoliki Waario. Kumbe alipohutubia umati, akashangiliwa na pande zote mbili, "Ambrosi askofu! Ambrosi askofu!". Alitaka kukataa, kwa kuwa hata hajabatizwa, lakini hatimaye alikubali ambapo inasemekana kuwa ni tarehe 7 Desemba ambayo ndo tarehe alipopewa ubatizo,kipaimara na ekaristi, halafu baada ya wiki moja daraja takatifu ya uaskofu na baadae aliwapatia Kanisa na mafukara dhahabu na fedha zake zote.
Kati ya mambo ya pekee aliyoacha ni urithi wa tenzi na liturujia ya pekee inayoendelea kutumika Milano na sehemu nyingine kadhaa za Italia kaskazini na Uswizi ("liturujia ya Kiambrosi"). Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.Sikukuu ya Mtakatifu Ambrosi wa Milano inaadhimishwa kila mwaka tarehe 7 Desemba.
Baba yake na Mtakatifu Ambrosi wa Milano, aliitwa Ambrosius Aurelianus, na alikuwa liwali wa Gallia; mama yake alijulikana kwa akili na imani yake. Ndugu wa Mtakatifu Ambrosi wa Milano ni, Satiro na Marselina wanaheshimiwa pia kama watakatifu.
Mtakatifu Ambrosi wa Milano alipofiwa na baba yake, alihamia Roma pamoja na mama aliyemuandaa kufuata nyayo za baba yake katika siasa. Alisomea huko, hasa fasihi,sheria na hotuba.Liwali Anicius Probus
kwanza alimpa nafasi katika halmashauri halafu mwaka 370 akamfanya gavana wa Liguria na Emilia, akiwa na makao makuu huko Milano, na mji wa pili wa nchini Italia
Kama askofu, zaidi ya useja wake, alishika juhudi za kitawa, alisaidia mafukara kwa mali zake karibu zote, akajitahidi kupata elimu ya Biblia na teolojia hasa kutoka vitabu vya Origene akaitumia vema katika kuhubiri, akifafanua kwa upana na udhati maandiko matakatifu alivyoyatafakari kwanza. Hivyo alieneza magharibi mtindo wa Lectio Divini ulioanzishwa na mtaalamu huyo wa Misri.
Augustino aliandika kwamba kila alipokwenda kumuona Ambrosi alimkuta amefikiwa na umati wa watu wenye shida mbalimbali, ambao alijitahidi kwa kila namna kuwasaidia. Kila mara kulikuwa na foleni ndefu ikisubiri kuongea naye ili kupata faraja na tumaini . Akibaki kidogo peke yake, alilisha au mwili kwa kula au roho kwa kusoma.
Mwenye nguvu na uadilifu, pamoja na kipawa cha kuhisi nini inawezekanika, aliweza kuongoza jimbo vizuri ajabu kama mchungaji halisi, mwenye msimamo na busara, na hasa wema na upendo. Hivyo hakufukuza wakleri waliofuata mafundisho ya Ario.
Mwaka 378 alikutana na Kaisari Grasyano, aliyemuomba amfundishe imani kinyume na mafundisho ya Ario. Baadaye Kaisari huyo alizidi kusimama upande wa Wakatoliki akatoa hati dhidi ya wazushi tarehe 22 Aprili 380, halafu akaieneza kwa Wapagani, akiwaondolea fadhili zao za awali.
Mwaka uliofuata wote wawili walishiriki mtaguso wa Aquileia ili kuimarisha imani sahihi katika dola.
Baada ya Grasyano kuuawa mwaka 383, ilimbidi Ambrosi azidi kupambana na wafuasi wa Ario, mmojawao akiwa Kaisari Masimo aliyedai mwaka 386 awaachie makanisa mawili ya Milano. Ambrosi alikataa katakata, akisema, "Ukinitaka mwenyewe, niko tayari kutii: unipeleke gerezani au kifoni, sitapinga; lakini sitasaliti kamwe Kanisa la Yesu Kristo. Sitaita watu kunisaidia; nitakufa kwenye altare lakini si kuikimbia. Sitahimiza watu kupiga kelele lakini Mungu tu anaweza kuwatuliza". Hivyo alihamia pamoja na wafuasi wake basilika lililogombaniwa wakaendelea kulitumia usiku na mchana.
Kadiri ya Augustino, aliyeguswa sana na umoja huo, ndiyo mwanzo wa nyimbo za Ambrosi: “Umati wenye imani ulikesha, ukiwa tayari kufa pamoja na askofu wao… Sisi pia, ingawa vuguvugu kiroho, tulishiriki katika mhemko wa wote”..
Ikulu haikupendezwa na msimamo wa Ambrosi, lakini ilimuogopa na kumhitaji katika mapambano ya siasa. Mahusiano yaliendelea kuwa magumu.
Hatimaye Theodosius I, Kaisari wa Mashariki, alipoangamiza mwaka 390 watu 7,000 huko Thesalonike nchini Ugiriki, Ambrosi alitisha kumtenga na Kanisa asipofanya toba kama mfalme Daudi, akamruhusu kupokea tena ekaristi baada tu ya miezi kadhaa ya malipizi.
Mtetezi wa wale wote walionyanyaswa, alipambana vilevile na seneti ya Roma na malkia ili kutetea siasa ya Kikristo kweli.
Msimamo wake ulibaki kielelezo kwa Kanisa la Magharibi hata likaendelea kudai uhuru na mara nyingi kushindana na mamlaka za serikali zisizotenda haki.
Ambrosi alipaswa pia kupambana na Wapagani waliotaka kufanya tena dini ya jadi kuwa dini rasmi ya Dola la Roma badala ya Ukristo. Alifaulu kumfanya Theodosius I atoe hati zake maarufu za mwaka 391.
Mtume wa upendo, alisaidia yeyote aliyemkimbilia, hata akauza vyombo vya ibada ili kukomboa watumwa , akisema, “Ikiwa Kanisa lina dhahabu, si kwa ajili ya kuitunza, bali ili liwape wanaohitaji”.
Tarehe 4 Aprili, siku ya ijumaa Kuu, Ambrosi alifariki huku amenyosha mikono yake kama Yesu msalabani, akaheshimika mara kama mtakatifu.
Masalia yake, ambayo ni kati ya maiti za zamani zaidi zilizopo nje ya Misri, yanatunzwa katika kanisa lake mjini Milano.
Sala yake
Ee Bwana, mwenye huruma kwa wote, uniondolee dhambi zangu, na kwa huruma washa ndani mwangu moto wa Roho wako Mtakatifu.Uniondolee moyo wa jiwe na kunipa moyo wa nyama, moyo wa kukupenda na kukuabudu wewe, moyo wa kupata raha ndani yako, kukufuata na kukufurahia kwa ajili ya Kristo.
Click here for reading more:
No comments:
Post a Comment