Kwa maana hiyo kumbe mtakatifu Fransisko wa Asizi hakupata mwanamke yeyote wa kumfuata kwa walau miaka sita tangu aongoke, na hata baada ya kumpata Klara, hakuwapata tena wengi.Sababu ni kwamba hakuwa mchungaji wa roho bali mtu mwenye kutafuta njia yake, wala hakuwa na mpango wa kuanzisha lolote, bali alitaka kushiriki tu hali ya watu wa mwisho.
Basi, kwa wanawake nafasi ya mwisho haikuwa tu ile ya wakoma, bali pia ya makahaba na ya wachawi.
Hivyo kwao chaguo la nafasi ya mwisho lilikuwa gumu zaidi, si tu upande wa mateso bali pia upande wa dharau, mbali ya kwamba lingesababisha masingizio juu ya uhusiano wao na ndugu wa kiume kama inavyosemekana.
Mtakatifu Klara alizaliwa mwaka 1193 au upande mwingine inasema ilikuwa 1194, hivyo alikuwa na miaka 12-13Mtakatifu Fransisko alipovua utu wa kale mbele ya mji mzima katika uwanda wa kanisa kuu ule ambako iko nyumba yaMtakatifu Klara.
Mtakatifu Klara wa Asizi aliendelea kusikia habari mbalimbali juu ya Mtakatifu Fransisko: alivyopata wafuasi, mmojawao Rufino binamu wa Klara; alivyokubaliwa na Papa n.k.
Haijulikani vyema kama ni kwa sababu hizo kwamba alikataa ndoa mbalimbali mpaka akafikia umri wa miaka 18, wala hatujui kama walikutana mara nyingi kwa mashauri ya kiroho.
Ila inajulikana kwa hakika kuwa baada ya Mtakatifu Klara kukimbia nyumbani usiku na kujiunga na jamaa ya ndugu wadogo, akifuatwa na mdogo wake Anyesi baada ya wiki mbili tu,Mtakatifu Fransisko alitimiza wajibu wa kumlisha kiroho kwa mahubiri, mifano na hata maandishi.
Kwa ushahidi wa Mtakatifu Klara tunajua kwamba hata kwake himizo kuu la Mtakatifu Fransisko lilikuwa kuambatana moja kwa moja na ufukara wa Mwana wa Mungu.
Mapema sana (kabla ya mwanzo wa mwaka 1213)Mtakatifu Fransisko aliwaahidia akina Klara kuwashughulikia sawa na ndugu wa kiume, akafanya hivyo mpaka kufa, ingawa kipindi fulani alijizuia asiwatembelee kusudi ndugu wengine wasipate kisingizio cha kufanya hivyo.
Mtakatifu Klara aliitikia kwa namna bora ya upendo na uaminifu, akamsaidia kuelewa vizuri zaidi wito wake wa kitume.Kufika kwake kwenyewe kulimfanya Fransisko afikirie sana na kushauriana naye juu ya maisha atakayoyashika.
Mara wakatambua njia ya wanawake iwe tofauti na ile ya wanaume: kwa hiyo Mtakatifu Klara akawa mmonaki na baadaye apesi, ingawa kwa kushika kikamilifu ufukara mkuu na kuhusiana kidugu na wenzake.
Tofauti na Ndugu Wadogo, ambao Mtakatifu Fransisko aliwaelekeza wafuate “mtindo wa Injili takatifu”, yaani Yesu alivyowaagiza mitume waende (Math. 10:5-15), aliwaelekeza Waklara kwenye “ukamilifu wa Injili takatifu”, unaoonyeshwa hasa na heri nane na hotuba nzima ya mlimani (Math. 5:1-7:27), bila ya kuwabana kwa mtindo huo wenye vipengele vingi vya pekee.
Tofauti inaonekana kuwa wazi katika ushahidi wa Askofu Yakobo wa Vitry ulioandikwa mwaka 1216 ukieleza maisha ya Wafransiko yalivyokuwa bado mwanzoni: wote walikuwa wanakula jasho lao, ila ndugu wa kiume kwa kufanya kazi hasa mjini au vijijini, kumbe akina dada kwa kubaki katika makao yao.
Mtakatifu Fransisko aliwahurumia daima wanawake hao waliokubali dharau na magumu ya kila aina.
Yeye, ambaye hakusita hata kidogo kufuata tu mtindo wa Injili, katika kuwaongoza alizingatia sana udhaifu wa jinsia yao, na kama kwa kulazimishwa tu na Mtakatifu Klara alimruhusu kushika magumu mengi: kila mara huruma ya Fransisko na msimamo imara wa Klara vilikutana katika kumpendeza Mungu.
Ni baada tu ya kung’amua msimamo huo, kwamba Fransisko alimuahidia atawatunza sawa na ndugu wa kiume.
Mwongozo wake wa uso kwa uso ukawa muhimu kuliko kuwaandikia kanuni fulani: badala yake mwenyewe alichukua jukumu la kudumisha ufukara mkuu na udugu katika monasteri ya kike.
Inasemekana baada ya kifo cha Mtakatifu Fransisko, akina Klara waliweza kushuhudia madonda ya Yesu katika mikono, miguu na ubavu wa mtakatifu huyo.Halafu wakaendelea kupigania ufukara mkuu dhidi ya mashauri ya watu mbalimbali.
Ni a zaidi ni kwamba baada ya Mtaguso IV wa Laterano (1215) kukataza kanuni mpya iliwabidi wapokee mojawapo ya zamani ili wakubaliwe na Kanisa Katoliki kama watawa. Basi wakaichagua ile ya Benedikto wa Nursia, wakiifuata katika mambo kadhaa kadiri yalivyopatana na mtindo wao mpya, bila ya nia ya kuwa Wabenedikto.
Hapo ilimpasa Klara kuitwa abesi, jina alilolikubali tu kwa kumtii mwanzilishi, ingawa akaendelea kujiita “mtumishi wa Kristo na wa akina dada fukara”.
Hasa Klara hakutosheka na uhalali wa monasteri yake mbele ya Kanisa, bali kwa njia ya Fransisko aliomba akapewa na Papa Inosenti III “fadhili ya ufukara” (1216), yaani ruhusa ya kuishi bila ya mali hata kijumuia, kama jambo la msingi katika wito wake wa “kuishi kadiri ya Ukamilifu wa Injili takatifu”, kwa kuungana na Yesu fukara kama bibiarusi fukara.
Kardinali Ugolino, akiona monasteri za namna hiyo zinavyoongezeka huko na huko, alizitungia katiba (1219) iliyopitishwa na Papa Honori (1216-1227) ambayo ikawa msingi wa kanuni zote zilizoandikwa baadaye kwa Utawa II.
Lengo lake lilikuwa kukinga monasteri hizo dhidi ya upinzani na kuzipa mtindo wa kimonaki zaidi bila ya kuondoa usahili wake maalumu, ziwe muundo mpya wa aina moja chini ya Kanisa la Roma moja kwa moja.
Katika juhudi zake za kurekebisha umonaki alielekeza hata monasteri kadhaa za zamani zifuate mtindo wa Mt. Damiano.
Desturi kali alizoziagiza humo hazikumtisha Klara, ambaye alijishinda tayari na kujitesa kwa ushujaa mkubwa (katika kula, kuvaa, kulala n.k.) mpaka akakatazwa asizidishe.Wala hakuogopa ukali wa ugo ulioagiwa na katiba hiyo, ili kutunza mazingira ya sala.Wasiwasi wake ulihusu ufukara mkuu akiona hautajwi na katiba hiyo.
Mwanzoni Ugolino alitaka msimamo huo udumu katika monasteri kadhaa, ila alipochaguliwa kuwa Papa akaanza kuzipatia mali nyinginyingi, labda kisha kung’amua matatizo yaliyojitokeza.
Lakini Klara hakukubali kabisa akamuomba amtibitishie “fadhili ya ufukara” akakubaliwa (1228), lakini si kwa monasteri zote.
Suala lingine lililojitokeza mapema, halafu likaendelea kusababisha migogoro, ni nani awajibike kuwasaidia Waklara upande wa roho na upande wa riziki.
Mtakatifu Fransisko alipokuwa Mashariki ya Kati, Filipo Longo aliteuliwa msimamizi wao, lakini mwanzilishi aliporudi uteuzi huo ukafutwa, masista wakasimamiwa tena na wasio Wafransisko, mpaka Ugolino, kisha kuchaguliwa awe Papa Gregori IX kuanzi mwaka 1227-1241 alipowalazimisha Ndugu Wadogo kuwajibika
Mtakatifu Klara alipoona wito wake wa Kiinjili upo hatarini upande wa sheria, kwa kuwa kanuni na katiba hazikuwa za Kifransisko, akaanza kuomba aweze kuahidi kushika kanuni ya Ndugu Wadogo badala ya ile ya Benedikto.
Mwaka 1234 akaja kumuunga mkono Anyesi wa Praha, binti mfalme ambaye alikataa kuolewa na mfalme mkuu Federiko II wa Ujerumani akaanzisha monasteri yake iliyokubaliwa “fadhili ya ufukara”.
Alitunga kanuni mpya kwa kuchanganya “mtindo wa maisha” alioandika Fransisko na katiba ya Ugolino, akamuomba Gregori IX, halafu Papa Inosenti IV Toka mwaka (1243-1254) waithibitishe, lakini akakataliwa.
Kumbe Papa Inosenti IV akathibitisha katiba ya Ugolino (1245) na kusisitiza ifuatwe kanuni ya Benedikto kwa sababu ina sifa nyingi.
Wakati huohuo alijaribu kusuluhisha mgogoro wa uhusiano kati ya Ndugu Wadogo na Waklara.
Klara alikuwa akiendelea kudai kwa nguvu msaada wa kiroho wa ndugu hao kulingana na ahadi ya mwanzilishi.
Kumbe Mtumishi mkuu Kreshensi wa Iesi (1244-1247) aliomba shirika liondolewe mzigo liliobebeshwa na Gregori IX, yaani himizo la kuanzisha koventi ndogo karibu na kila monasteri ya Waklara.
Basi, Inosenti IV aliamua Waklara wawe chini ya uongozi na mamlaka ya Ndugu Wadogo, akapendekeza masista waunganishwe na Utawa I.
Lakini shirika likazidi kuona litalemewa na wingi wa monasteri.Mwaka 1247 Papa Inosenti IV akatunga katiba mpya badala ya ile ya Ugolino iliyokwishaenea katika monasteri zote za Kifransisko, ikitumika pengine pamoja na desturi maalumu za mahali.
Katiba hiyo ilifanya kanuni ya Ndugu Wadogo kuwa msingi wa sheria za Waklara bila ya kuwadai waishike katika yote, ila katika utiifu, utovu wa mali na useja utakatifu.
Katiba hiyo ilimuondolea Kardinali mlinzi mamlaka juu ya Waklara, ambao wakawekwa moja kwa moja chini ya viongozi wa Utawa I.
Kwa katiba hiyo Waklara wakaja kutambulikana Wafransisko kisheria, lakini ndani mlikuwa na pigo kubwa kwa Klara, yaani iliandikwa wazi kuwa monasteri zao zinaruhusiwa kuwa na mali za kujitegemea.
Ndiyo sababu monasteri chache tu zikaipokea katiba hiyo.
Vilevile Ndugu Wadogo wakazidi kulalamika hadi Kardinali mlinzi akajitwalia polepole mamlaka yao na hatimaye mwaka 1250 aliwaandikia wasithubutu kujiingiza katika uongozi wa Waklara.
Hivyo kwa muda mfupi katiba hiyo ikashindikana pande zote.
Klara, mgonjwa toka siku nyingi, alipoona kifo kinamkaribia, aliandika wasia wake ambamo alimuiga Fransisko katika kukumbusha asili ya wito wake na wa jamaa yake, na kutamka kwa msisitizo mkubwa nia imara ya kufuata ufukara mkuu “aliouahidi kwa Mungu na kwa Mt. Fransisko” pamoja na kuhimiza sana umoja wa dada zake.
Lakini pia, upande wa sheria, aliona haja ya kutunga upya “mtindo wa maisha” kwa kulinganisha kanuni ya Ndugu Wadogo na masharti ya maisha ya ndani tu.
Humo aliingiza pia maandishi mawili mafupi ya Fransisko kwao, kuhusu ufukara mkuu na kuhusu ahadi ya kwamba yeye na Ndugu Wadogo watawahudumia Waklara sawa na wenzao wa kiume.
Upande wake Klara aliahidi kuwatii waandamizi wa mwanzilishi. Kiini cha huo “mtindo wa maisha” kinasisitiza kwa nguvu nia ya kuishi bila ya mali yoyote, isipokuwa monasteri na bustani.
Jambo lingine linalokazwa ni udugu: humo neno “dada” linapatikana mara 66!
Udugu huo unatimizwa siku kwa siku chini ya “abesi na mama” kwa umoja wa mioyo pasipo ubaguzi wowote (tofauti pekee ni kati ya wanaojua na wasiojua kusoma kuhusu Sala ya Kanisa).
Hata dada “wa nje” (yaani “wanaohudumia nje ya monasteri” bila ya kubanwa na ugo) washiriki maisha ya jumuia sawa na wenzao.
Hao ni kundi maalumu la mtindo wa Kiklara, linalohitajika kadiri wenzao wanavyojifungia ndani: ni “akina Marta” kwa “akina Maria” kadiri Fransisko alivyowapangia Ndugu Wadogo wanaoishi upwekeni.
Udugu huo unajitokeza hata katika mikutano, ambayo inatakiwa kufanyika kila wiki kwa mchango wa wote, kupanga shughuli za maana na kuteua watakaoshika nyadhifa mbalimbali.
Abesi mwenyewe, ingawa anachaguliwa kwa maisha yake yote, kadiri ya mapokeo ya kimonaki, anaweza kubadilishwa na dada zake wakiona hawezi kutimiza vizuri kazi zake.
Uhusiano na Utawa I unasisitizwa tena kwa kudai msimamizi wa monasteri awe daima Ndugu Mdogo, pamoja na kuomba Utawa huo uipatie monasteri mapadri 2 na mabradha 2 kwa huduma za kiroho na za kimwili.
Huo “mtindo wa maisha” ukakubaliwa na Kardinali mlinzi mwaka 1252 halafu na Papa Inosenti IV mwaka 1253.
Mtakatifu Klara akapewa hati yake kitandani akaibusu; siku mbili baadaye akafa akiishika mikononi, wakihudhuria Leo, Anjelo na Yunipero, “wenzi watatu” wa Mtakatifu Fransisko; pia alijaliwa faraja za Bikira Maria na wanawake watakatifu kadhaa.
Baada ya kifo chake mazishi yalihudhuriwa na Papa, Makardinali, Maaskofu na wengineo.
Papa Inosenti IV alitaka ziimbwe sala za watakatifu mabikira badala ya zile za wafu, ila akakubali shauri la Kardinali mlinzi la kufuata taratibu zilizopangwa kabla mtu hajatangazwa mtakatifu.
Miaka miwili baadaye, Kardinali huyo akiwa amechaguliwa kuwa Papa Aleksanda IV mwaka 1245-1261, akamtangaza rasmi kuwa mtakatifu mwaka 1255.Na mwaka 1260 masalia yake yakahamishiwa mjini Asizi katika kanisa lililojengwa kwa heshima yake.
Siku yake inaazimishwa tarehe 11 Augost kila mwaka na anajulikana kwa kuheshimiwa na Kanisa Katoliki kama mtakatifu na msimamizi wa television.
vyanzo(https://sw.wikipedia.org/wiki/Klara_wa_Asiz)
for more reading:
No comments:
Post a Comment