Kanisa Kanisa la Mt. Peter Claver huko Cartagena,Kolombia , alipoishi na kufanya kazi.
Mtakatifu Peter Claver alizaliwa tarehe 26 June 1581 Verdu Catalonia,Hispania na alifariki katika mji wa Cartagena,Kolombia tarehe 8 Septemba 1654.Mtakatifu Peter Claver alikuwa padri mjesuiti mmisionari huko Amerika Kusini.
Mtakatifu Peter Claver anaheshimiwa kama msimamizi wa misheni zote za Kanisa Katoliki kwa watu wenye asili ya Afrika kwa sababu alijitoa kwa nadhiri ya kujifanya mtumwa wa watumwa.Inakadiriwa Mtakatifu Peter Claver aliwabatiza waumini 300,000 hivi katika kipindi cha miaka 40 ya kuhudumia Wanegro wa Kolombia kiroho na kimwili.
Mtakatifu Peter Claver alitangazwa kuwa mwenye heri tarehe 16 Julai 1851 na Papa Pius IX na baadae alifanywa kuwa Mtakatifu tarehe 15 Januari 1888 kwa kutangazwa na Papa Leo XIII.
Tangu kuzaliwa Kwake
Mtakatifu Peter Claver baada ya kuzaliwa kwake huo mwaka 1581 kwenye mji wa Verdu familia yao ilikuwa ya Kitajiri ya wakulima Wakatoliki wazuri ikiwa ni miaka 70 baada ya Mfalme Ferdinando wa Hispania kuanzisha biashara ya watumwa kwa kuruhusu ununuzi wa Waafrika 250 huko Lisbon kwa ajili ya makoloni yake ya Amerika.Biashara ya watumwa ilishamiri sana kwenye karne ya 17 kutoka Afrika kwenda Amerika. Kutokana na mazingira hayo Mtakatifu Peter Claver alijisikia kuongozwa na Mungu afanye kazi kwa juhudi zote.
Mtakatifu Peter Claver akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Barcelona inasemekana na akili nyingi na moyo wa upendo hasa watumwa. Baada ya kusomea huko miaka miwili, aliandika hivi katika daftari lake dogo alilolitunza maisha yake yote: "Natakiwa kujitoa nimtumikie Mungu hadi kifo, nikijifananisha na mtumwa."
Baada ya kumaliza masomo yake, Mtakatifu Peter Claver alijiunga na shirika la Yesu huko Tarragona akiwa na umri wa miaka 20. Kisha kumaliza unovisi, baadae alitumwa kusoma falsafa huko Palma Mallorca.Akiwa huko alifahamiana na bawabu wa chuo cha shirika, Mtakatifu Alfonso Rodriguez, bradha maarufu kwa utakatifu na kwa karama ya unabii. Rodriguez alijisikia ameambiwa na Mungu kwamba Peter Claver alitakiwa kutumia maisha yake katika makoloni ya Hispania Mpya barani Amerika, akamhimiza mara nyingi kuitikia wito huo.
Mtakatifu Peter Claver alijitolea kwenda na kutumwa katika ufalme wa Granada Mpya , alipofikia katika bandari ya Cartagena mwaka 1610. Mtakatifu Peter Claver alitakiwa kusubiri miaka 6 kabla ya kupewa upadrisho wakati wa kusoma teologia , aliishi katika nyumba za Wajesuiti huko Tunja na Bogota. Katika miaka hiyo ya maandalizi, aliguswa sana na ukali uliotumika dhidi ya watumwa, pamoja na hali yao ngumu kwa jumla.
Cartagena ilukuwa kituo cha biashara ya watumwa. Kwa mwaka watu 10,000 walikuwa wanashushwa bandarini kutoka Afrika Magharibi baada ya kusafirishwa melini katika hali ya kutisha, kiasi kwamba inakadiriwa thuluthi moja walikuwa wanakia njiani. Ingawa biashara hiyo iliharamishwa na Papa Paulo III Na Urban VIII faida yake kiuchumi ilifanya iendelee kustawi
Mtangulizi wa Peter Claver katika utume wake wa moja kwa moja, padri Alonso de Sandoval, S.J., alimuandaa na kumuongoza hata kwa mfano wake. Sandoval alimuona Peter Claver kuwa mwanafunzi bora. Mwenyewe alikuwa amehudumia watumwa kwa miaka 40 kabla Mtakatifu Peter Claver hajafika kumpokea katika kazi hiyo. Sandoval alikuwa amejitahidi kujifunza desturi,ibada na lugha za Waafrika, akafaulu kiasi cha kuweza kuandika kitabu juu ya hayo mwaka 1627 baada ya kurudi Seville.
Mtakatifu Peter Claver alipoweka nadhiri za daima mwaka 1622 katika shirika , alisaini hivi kwa Kilatini hati ya kujiweka wakfu : Petrus Claver, Aethiopum semper servus ikiimanisha hivi: Petro Claver, mtumwa wa kudumu wa Waafrika.
Inasemekana Sandoval alikuwa akiwatembelea watumwa mahali pa kazi zao kumbe Mtakatifu Peter Claver aliona afadhali kuwasubiri bandarini na kupanda mara kwa mara melini kuwahudumia walionusurika katika safari ingawa ilikuwa shida kutembea kati ya kwa jinsi walivyobanana.
Baada ya kushushwa ili kupangwa sokoni na kuuzwa baada ya umati wa wanunuzi kuwachunguzachunguza, Mtakatifu Peter Claver alikuwa anawapatia dawa,chakula,kileo,limau na tumbaku. Kwa msaada wa wakalimani na picha kubwa aliyoleta, aliwapa mafundisho ya msingi katika imani ya Ukristo.
Mtakatifu Peter Claver alishindana na baadhi ya Wajesuiti wenzake waliokubali utumwa, akahimiza wote kuwaona watumwa kama ndugu katika Kristo. Baada ya kuwafundisha na kuwabatiza alijitahidi wapate haki zao kama binadamu na kama Wakristo .Hata hivyo utume wake ulienea zaidi, kwa kuhubiri barabarani kwa mabaharia na wafanyabiashara pamoja na kwenda vijijini mpaka wakati wa kurudi kuwatembelea aliowabatiza na kuwatetea.Wakati wa safari hizo, alikuwa anajitahidi kukwepa mapokezi ya wenye mashamba na wanyapara wao, akipendelea kulala katika makazi ya watumwa.
Vilevile alihudumia waliotembelea Cartagena na waliohukumiwa adhabu ya kifu , ambao amewaandaa wengi kufa vizuri kiroho; pia alitembelea mara nyingi hospitali za mji huo.
Mtakatifu Peter Claver inasemekana mwaka hadi mwaka, kazi na ushuhuda wake vilileta nafuu fulani katika hali ya watumwa, naye akawa na sauti iliyosikika.Miaka ya mwisho,Mtakatifu Peter Claver alikuwa mgonjwa mno asiweze kutoka chumbani. Kwa miaka 4 alibaki karibu peke yake, akihudumiwa vibaya (hata karibu kuachwa bila chakula) na mtumwa aliyekombolewa ambaye mkubwa wa nyumba alimuagiza kumshughulikia.Mtakatifu Peter Claver hakulalamika kamwe, alikubali yote kama malipizi ya dhambi zak.
Inasemekana watu wa Cartagena walipopata habari ya kifo chake hiyo tarehe 8 September 1654,walilazimisha waruhusiwe kuingia chumbani ili kumpa heshima ya mwisho. Kutokana na sifa zake, walijipatia vipande vya nguo zake kama masalia hata karibu kumuacha uchi.
Wakuu wa mji, ambao awali walimuona anawasumbua daima kwa kutetea watumwa, waliagiza mazishi ya fahari.
Mtakatifu Peter Claver alitangazwa mtakatifu pamoja na Alfonso Rodriguez, na baada ya miaka minane Papa Leo XIII alimtangaza mwaka 1896 kuwa msimamizi wa umisionari wote katika ya Waafrika.
Mwili wa Mtakatifu Peter Claver unatunzwa katika Kanisa la Wajesuiti alipokuwa anaishi, ambayo sasa linaitwa kwa jina lake.
No comments:
Post a Comment